LOWASA SPEECH

Dar es Salaam. Kada mpya wa Chadema, Edward Lowassa jana alichukua tena fomu ya kuwania urais lakini safari hii si kwa tiketi ya CCM, katika hafla ambayo ilishuhudiwa na umati mkubwa wa watu uliosababisha Mtaa wa Ufipa kufungwa kwa saa tatu.
Hafla hiyo pia ilitawaliwa na matukio mengi, likiwamo la waziri huyo mkuu wa zamani kuanza rasmi kutumia kaulimbiu ya Chadema ya People’s Power huku akinyoosha juu mkono uliokunja ngumi na kusababisha umati huo kulipuka kelele za shangwe.
Lowassa, ambaye Jumanne wiki hii alitangaza rasmi kujiondoa CCM na kujiunga na Chadema, alikabidhiwa fomu ya kugombea urais na mwenyekiti wa chama hicho, Freeman Mbowe, ambaye alifanya kazi hiyo badala ya Katibu Mkuu, Dk Willibrod Slaa ambaye kwa mara nyingine hakuonekana kwenye tukio kubwa la chama hicho.
Katika hafla hiyo fupi, Lowassa ambaye wanachama walimchangia Sh1 milioni kwa ajili ya kuchukua fomu za kuwania urais, alitumia dakika nne kuzungumza, huku akiwashukia wanaomshambulia kuwa kujiunga kwake Chadema kunatokana na uroho wake wa madaraka.
“Wanapoteza muda na hawataniyumbisha,” alisema mbunge huyo wa Monduli.
Lowassa, aliyekuwa amevaa shati jeupe na suruali nyeusi na aliyekuwa kwenye gari aina ya Toyota Land Cruiser VX, alifika makao makuu ya Chadema saa 6:40 mchana akiwa pamoja na mkewe, Regina na familia yake na alipokewa na umati mkubwa wa watu waliokuwa wakiimba “rais, rais, rais… tuna imani na Lowassa, oya oya oya”.
Mara baada ya kushuka, Lowassa aliwapungia watu hao mkono huku akitabasamu, hali iliyosababisha kila mtu kutaka kumshika mkono jambo ambalo liliwapa wakati mgumu walinzi wa chama hicho, wanaojulikana kwa jina la Red Brigade.
Mbali na familia yake, Lowassa alisindikizwa na mbunge wa Arumeru Magharibi (CCM), Goodluck Ole Medeye na kada mkongwe wa CCM, Madson Chizii.
Watu wa rika mbalimbali walijaa kwenye ofisi za makao makuu ya chama hicho zilizopo Mtaa wa Ufipa na baadhi walitumia simu za mkononi kuchukua picha za tukio hilo.
Hali hiyo ilisababisha mtaa huo kufungwa huku wenye magari wakitakiwa na walinzi wa chama hicho kutafuta njia nyingine, kwa maelezo kuwa “rais wa nchi” anachukua fomu.
Wakati Lowassa akiwa ndani, watu hao waliendelea kushangilia na kuimba nyimbo mbalimbali nje ya ofisi hiyo, hasa walipomuona akizungumza na Tundu Lissu.
‘Yes We Can’
Katika hotuba yake Lowassa, alisema wakati wa kuing’oa CCM ni sasa na kutumia kaulimbiu ya “Yes We Can (Ndio Tunaweza)” iliyotumiwa na Rais wa sasa wa Marekani, Barack Obama wakati akiomba kura za Wamarekani kwa mara ya kwanza kuongoza nchi hiyo.
“Nashukuru kwa mapokezi mliyonipa ninawashukuru walionichangia fedha za kuchukua fomu. Ninafurahi kwa heshima mliyonipa, heshima hii haina maelezo ya shukrani kusema nashukuru tu haitoshi ila kazi nitakayowatendea ndiyo itakuwa shukrani,” alisema Lowassa ambaye alijiuzulu uwaziri mkuu mwaka 2008.
“Najiandaa kufanya kazi iliyotukuka na itakayotuletea ushindi sisi (Chadema) na Watanzania.”
Lowassa aliwataka wananchi kujiandikisha katika daftari la wapigakura ili waweze kumchagua kiongozi wanayempenda.
“Mliojiandikisha mnatakiwa kutunza shahada zenu kungoja tarehe ya uchaguzi. Uchaguzi huu utakuwa ni namba tu (wingi wa kura), kama alivyosema (mwanasheria wa Chadema, Tundu) Lissu kuhusu kushinda ubunge na urais. Tunaweza kupata kura hizo mimi nina uhakika huo,” alisema.
Alisema anachokifanya sasa ni kutekeleza maelezo ya Mwalimu Julius Nyerere kuwa Watanzania wasipoyapata mabadiliko ndani ya CCM, watayatafuta nje ya chama hicho. “Mimi nimeridhika kwamba ndani ya CCM mabadiliko hayo hayawezekani kupatikana, lakini nimeridhika kuwa Watanzania wanataka mabadiliko na watayapata kwa kura zetu. Watanzania wanaotaka mabadiliko ni wengi naamini tukijipanga vizuri tutashinda uchaguzi huu bila matatizo yeyote,” alisema.
Alisema ushindi huo utapatikana bila kutumia lugha za matusi, kejeli na kwamba ustaarabu na kutoa hoja za msingi ndio chachu ya ushindi huo.
“Rais Barack Obama alipokuwa akigombea urais kwa mara ya kwanza aliwauliza wenzake ‘can we (tunaweza)?’, wakamjibu ‘yes we can (ndio tunaweza)’. Na mimi nataka kuwambia wenzangu ndio tunaweza,” alisema.
Kauli ya kuunganisha Chadema
Kabla ya Lowassa kuzungumza, Mbowe alisema kuwa kada huyo wa zamani wa CCM hawezi kueleweka kwa wanachama iwapo hatasema kaulimbiu ya chama hicho ya People’s Powe, inayomaanisha Nguvu ya Umma, akisema ndiyo inayowaunganisha wana-Chadema.
Baada ya Lowassa kutamka neno hilo, alishangiliwa na watu waliojazana eneo hilo ambao walimtaka arudie. Baadaye Mbowe alisema sasa amekuwa kamanda rasmi ndani ya chama hicho kikuu cha upinzani nchini.
“Tunaendelea kuwa pamoja kuandika historia,” alisema Mbowe. “Naomba kuwahakikishia jambo moja la msingi, Chadema ni chama makini na kitaendelea kuwa chama makini chenye kusheshimu, katiba, kanuni na maadili yake.”
Akizungumzia vikao vya kikatiba vya chama hicho, Mbowe alisema Agosti 2 kitafanyika kikao cha Kamati Kuu ambacho kitaanza kujadili fomu za mgombea na Agosti 3 kutakuwa na mkutano wa Baraza Kuu ambalo pamoja na mambo mengine litachambua ilani ya chama kuelekea uchaguzi mkuu, ushirikiano wa vyama vinavyounda Ukawa na kuchambua fomu za mgombea urais.
Alisema Agosti 4 utafanyika Mkutano Mkuu ambao utapitisha jina la mgombea urais na mgombea mwenza pamoja na Ilani ya Uchaguzi ya Chadema, na ilani ya uchaguzi ya vyama vinavyounda Ukawa ambavyo ni NCCR-Mageuzi, Chadema, NLD na CUF.
Agosti 5, 6 na 7 Kamati Kuu itakutana mfululizo kuchambua na kuidhinisha wagombea ubunge kwa niaba ya Chadema, akisema vitafanya kazi kwa umakini kwa kuwa Chadema inajiandaa kuongoza dola.
Lissu
Akizungumzia mchakato uliotumika kumpata mgombea mwenye sifa, Lissu alisema ilifanyika kazi kubwa.
“Tumefanya hivyo kwa sababu tunataka Oktoba 25 iwe ndiyo mwisho wa utawala wa zaidi ya nusu karne wa CCM na mfumo wao wa utawala. Tumefanya utafiti wa kina na mpaka kupata jina la Lowassa,” alisema.
Alisema utafiti wa miezi mitatu wa Kamati Kuu ulihusisha viongozi wote wakuu wa chama hicho na wajumbe wa kamati kuu na sekretarieti.
“Utaratibu wa kumpata Lowassa ulimhusisha katika hatua zote Mbowe, Dk Slaa, makamu wenyeviti wote wawili, naibu makatibu wakuu na wajumbe wote wa kamati kuu. Baada ya kazi hiyo kamati kuu ilikaa kikao Jumapili (Julai 26) na kufanya uamuzi kwamba Lowassa atapeperusha bendera ya Chadema,” alisema.
“Kwa mila na desturi za chama chetu, uamuzi unapofanywa na vyombo halali vya chama kwa kufuata njia zilizowekwa na katiba na kanuni kila kiongozi na mwanachama anapaswa kuheshimu na kutekeleza maamuzi hayo,” alisema.
Umati wa watu
Watu walianza kufika eneo hilo kuanzia saa 4:00 asubuhi na mpaka kufika saa 6:00 mchana mtaa wa Ufipa ulikuwa umefungwa kutokana na idadi kubwa ya watu.
Watu waliofika eneo hilo walionekana wavumilivu kusubiri ujio wake kwa saa tatu, kwani awali ilielezwa awali kuwa angewasili saa 5:00 asubuhi. Eneo hilo lilikuwa na vituo vya aina yake, hasa kijana aliyejitambulisha kwa jina la Juma David ‘Ngosha’ aliyekuwa amevaa sare za kijani zinazotumiwa na CCM na ambaye baadaye alichangiwa fedha ili anunue sare zinazotumiwa na Chadema.
Alipoulizwa sababu za kwenda eneo hilo na sare za CCM alisema: “Nilitaka kupima jazba ya watu, nilitaka kuona mapokeo yao.”
Wakati Lowassa akiondoka eneo hilo, mtu aliyekuwa amevalia sare zinazotumiwa na CCM alibebwa juu juu na kuwekwa chini ya ulinzi mkali kabla ya kupewa sare za Chadema, kisha kuzipokea na kuzivua sare za chama hicho tawala.
Sare zinazotumiwa na Chadema ziliuzwa kwa wingi eneo hilo.
“Hali ya kisiasa sasa imekuwa na manufaa makubwa kwetu,” alisema mmoja wa wauzaji hao, Ester Rwambano.
Dk Slaa, Mnyika wakosekana
Lakini shamrashamra hizo zilifanyika bila ya kuwapo kwa Dk Slaa, ambaye pia alikosekana Jumanne wiki hii wakati wa kumtambulisha Lowassa, na pia Naibu Katibu Mkuu Bara, John Mnyika.
Hakuna taarifa zilizotolewa kuhusu kutokuwapo kwao, ingawa Lissu, ambaye pia hakuwapo kwenye kikao cha kwanza alijizungumzia akisema kuwa bado yupo na ataendelea kuwapo.
Ole Medeye yupo Chadema ‘kiana’
Kwenye shughuli hiyo pia alikuwapo mbunge wa Arumeru Magharibi, Goodluck Ole Medeye, ambaye alieleza kuwa anahudhuria shughuli hiyo kwa kazi maalum.
 “Mimi ni mshauri wa Lowassa katika masuala ya kupambana na rushwa,” alisema. Alisema alijiondoa katika mchakato wa ubunge wa CCM baada ya kubaini unaendeshwa kwa rushwa.
 “Mchakato wa Chadema bado unaendelea, tusubiri ila siwezi kusema kama nipo Chadema,” alisema.
Dk Slaa mafichoni
Jitihada za kumtafuta Dk Slaa hazikuzaa matunda licha ya gazeti hili kufika nyumbani kwake, Mbweni na kuweka kambi kwa zaidi ya saa tatu.
Wakati waandishi wetu wakiendelea kumsubiri Dk Slaa, gari la Mbunge wa Kawe (Chadema), Halima Mdee lilipita karibu na makazi ya kiongozi huyo (Dk Slaa) na alipoulizwa alipo alijibu: “Dk yupo honeymoon (fungate), hana neno, anasubiri tuchukue nchi, amepumzika.”
Mdee pia alijibu tetesi za Dk Slaa kujiuzulu mara baada ya Lowassa kujiunga na chama hicho na kusema: “Hana matatizo kuhusu hilo na yupo vizuri.”
Mlinzi wa nyumbani kwa Dk Slaa aliyefahamika kwa jina moja la Abel alisema tangu migogoro ianze, kiongozi huyo wa Chadema na mkewe, Josephine Mushumbusi, wamekuwa mafichoni na kukataa kuzungumza na wanahabari. Alipoulizwa ni migogoro gani hiyo, alikataa kufafanua.

Comments

UNITEC COMPUTER ACCESS