Rais wa Jamhuri wa Muungano wa Tanzania, Jakaya Kikwete akutana na UKAWAK
25th August 2014
Rais Mstaafu Benjamin Mkapa
Wakati Rais Jakaya Kikwete akishinikizwa na makundi
mbalimbali ya kijamii yakimtaka kusitisha kwa muda Bunge Maalum la
Katiba, Rais Mstaafu Benjamin Mkapa, amejiweka mbali kabisa na Bunge
hilo na mchakato wa Katiba, akiweka wazi kuwa hatazungumzia vitu hivyo.
Mkapa alisema hayo wakati wa kumkaribisha Waziri Mkuu Mizengo Pinda,
katika hafla ya chakula cha jioni ya harambee ya Taasisi ya Benjamin
William Mkapa Hiv/Aids (BMAF), mradi wa Mkapa Fellows, jijini Mwanza
juzi.
“Sitaki kuzungumzia suala la Katiba Mpya wala mchakato wake unavyoenda,” alisema kwa kifupi Mkapa.
Ingawa Mkapa hakuwa ametakiwa kuzungumzia mchakato wa Katiba mpya wala
Bunge Maalum la Katiba katika hafla hiyo, aliamua kuchomeka maneno hayo
ya utangulizi pengine kujiweka mbali na mjadala wa katiba unaoendelea
nchini kwa sasa.
Kadhalika halfa hiyo ambayo ilikuwa imejaa wanasiasa, akiwamo Waziri wa
Nchi Ofisi ya Rais (Uratibu na Uhusiano), Steven Wasira, Waziri wa Nchi
Ofisi ya Waziri Mkuu (Tamisemi), Hawa Ghasia, Naibu Waziri wa Uchukuzi,
Charles Tizeba na Naibu Waziri wa Afya na Ustawi wa Jamii, Steven Kebwe.
Wengine ni Mkuu wa Mkoa wa Mwanza, ambaye pia anakaimu mkoa wa Mara,
Everest Ndekiro, Mkuu wa Mkoa wa Shinyanga, Ali Rufunga, Mkuu wa Mkoa wa
Geita, Magalula Ali Magalula, na wabunge wa CCM kutoka majimbo ya Kanda
ya Ziwa.
Kutokana na uwapo wa wanasiasa hao, kulikuwa na hisia kwamba huenda
Mkapa angezungumzia mchakato huo, kwani umekuwa ukitawala mijadala mingi
ya wanasiasa kwa sasa nchini.
Bunge la Katiba limegawanyika tangu wabunge wanaounda Umoja wa Kutetea
Katiba ya Wananchi (Ukawa) wajiengue na kuapa kutorejea huko kwa kile
walichosema ni kuchakachuliwa kwa rasimu ya Katiba Mpya ambayo
iliwasilishwa na Mwenyekiti wa Tume ya Mabadiliko ya Katiba, Jaji Joseph
Warioba.
Ukawa unaoundwa na wabunge kutoka Chadema, CUF, NCCR-Mageuzi, NLD na DP,
umekuwa ukiishutumu hotuba ya ufunguzi ya Bunge hilo ya Rais Kikwete
kuwa ndiyo iliagiza kuchakachuliwa kwa rasimu hiyo.
Kutokana na kususia Bunge hilo, shinikizo limekuwa likielekezwa kwa Rais
Kikwete alisitishe kwa madai kuwa kinachojadiliwa kwenye bunge hilo
siyo Rasimu ya Katiba Mpya kama ilivyoandaliwa kutokana na maoni ya
wananchi yaliyokusanywa na Tume ya Madiliko ya Katiba.
Hata hivyo, wiki iliyopita Kamati Kuu ya Chama Cha Mapinduzi (CCM),
ilikutana mjini Dodoma na kuridhia Bunge la Katiba kuendelea na mchakato
wa kujadili rasimu hiyo.
Bunge Maalum la Katiba linaloendelea mjini Dodoma kwa sasa linaelezwa
kugubikwa na wajumbe kutoka CCM na wanafanya mabadiliko makubwa ya
Rasimu ya Katiba ili kukidhi matakwa yao ya kisiasa.
Miongoni mwa mambo ambayo yameleta kutokuelewa kwingi ni mabadiliko ya
kuondoa mfumo wa Muungano wa serikali tatu unaopendekezwa na Rasimu ya
Katiba Mpya na badala yake kuingiza serikali mbili.
Ukawa wamekwisha kuweka wazi kuwa watafanya maandamano na mikutano
mikubwa nchi nzima kuhamasisha wananchi waikatae katiba itakayotolewa na
Bunge hilo kwa kuwa ni batili.
MKAPA FELLOWS NA AFYA
Baada ya utambulisho huo, Mkapa alisema taasisi hiyo iliyoanzishwa 2006
imekuwa mstari wa mbele kuchangia juhudi za serikali kupitia miradi
mbalimbali inayolenga kuimarisha huduma za afya.
Alisema taasisi hiyo iliyoanzishwa kutokana na ushauri wa Rais wa zamani
wa Marekani, Bill Clinton, imesaidiana na serikali na wala si
kushindana katika kutoa huduma za afya hususani vijijini.
“Vijana wa taasisi hii wamefanya kazi nzuri kwani wameenda kufanya kazi
kule ambako watumishi wa serikali walikuwa hawataki
kwenda…tumeshirikiana vizuri na Wizara ya Afya na Ustawi wa Jamii,”
alisema Mkapa.
Mkapa alisema mradi mmojawapo unaotekelezwa na taasisi hiyo ni “Mkapa
Fellows” ukiwa ni wa miaka mitano (2013/17) katika halmashauri 15 za
mikoa ya Shinyanga, Kagera, Simiyu, Rukwa na Zanzibar.
AJIRA 156
Awali Ofisa Mtendaji Mkuu wa Taasisi hiyo, Dk. Ellen Mkondya-Senkoro,
alisema ofisi yao imeajiri watumishi 156 kwa ajili ya kufanyakazi katika
vituo vya tiba mikoa ya Kanda ya Ziwa.
“Kutokana na kuajiri watumishi hawa, pia tunatarajia kujenga vyumba vya
upasuaji 23 na wodi ya wajawazito ngazi ya vituo vya afya utakaoanza
Januari mwakani,” alisema Dk. Senkoro.
Alisema lengo la mradi huo kwa miaka mitano ni kuajiri wataalamu wa afya
180, kujenga uwezo wa wataalam wa afya katika masuala ya Ukimwi na
utoaji wa elimu kwa jamii.
Mwenyekiti wa Bodi ya Wadhamini wa BMAF, Balozi Charles Sanga, alisema
mradi wa Mkapa Fellows umefikia karibu asilimia 80 ya maeneo nchini na
kufanikisha mengi.
Alisema yaliyofanikishwa ni pamoja na utoaji wa ajira kwa wataalam wa
afya 1000 vijijini, ufadhili wa wanafunzi 700 wa kada ya afya na ujenzi
wa nyumba 310 za wafanyakazi wa afya katika wilaya 31.
PINDA APONGEZA
Pinda katika hafla hiyo alimshukuru na kumpongeza Mkapa kwa kuanzisha
taasisi hiyo ambayo inachangia jitihada za serikali kuimarisha huduma za
afya.
Alisema kazi nzuri inayofanywa na taasisi hiyo katika mikoa ya Kanda ya
Ziwa na sehemu nyingine, inaungwa mkono na serikali moja kwa moja.
“Lengo la mradi huu ni kuimarisha huduma za afya hasa mapambano dhidi ya
Ukimwi na kuimarisha afya ya mama na mtoto kupitia uimarishaji wa
rasilimali watu katika sekta ya afya hususani maeneo yenye mazingira
magumu,” alisema Pinda.
Aidha, alisema hafla ya uchangiaji wa mfuko huo unaotegemewa kugharimu
Sh. bilioni 15 kwa miaka mitano, tayari umefanikisha kukusanya Sh.
bilioni 4.9 mpaka sasa.
Katika harambee hiyo iliyokuwa na malengo ya kukusanya Sh. 500,000,000
ilifanikisha kupatikana kwa Sh. bilioni 1.383 zikiwa ni pesa taslimu na
ahadi.
Wakati huo huo, juzi asubuhi Waziri Mkuu alitembelea na kukagua ujenzi
wa uwanja wa ndege wa kisasa jijini Mwanza pamoja na kutembelea ujenzi
wa jengo la kimataifa la biashara linalojengwa kati ya makutano ya
Makongoro na Furahisha.
Comments
Post a Comment