JAJI J. WARIOBA
Dar es Salaam. Mawaziri wakuu wa zamani, Dk
Salim Ahmed Salim na Jaji Joseph Warioba wameonya kuwa hali ya
mgawanyiko, ubaguzi wa kidini, ukabila na ujimbo miongoni mwa wananchi
inatishia umoja na utulivu wa nchi iwapo hatua hazitachukuliwa.
Wakizungumza kwa nyakati tofauti katika mkutano wa
siku mbili wa mashauriano kuhusu amani na umoja nchini ulioandaliwa na
Taasisi ya Mwalimu Nyerere (MNF) jana, viongozi hao walisema misingi ya
amani na utulivu iliyojengwa nchini inastahili kulindwa.
Katika siku za karibuni, viongozi wa dini ya
Kikristo na Kiislamu walitofautiana katika ahadi ya Serikali kuingiza
Mahakama ya Kadhi kwenye Katiba, suala la Muungano likisababisha mjadala
mkali bungeni, huku kukiwa na mapigano ya mara kwa mara ya wafugaji na
wakulima.
Dk Salim, ambaye ni mwenyekiti wa bodi ya
wadhamini wa MNF, alisema Watanzania wengi wana wasiwasi kuwa amani,
umoja na utulivu uliopo hivi sasa nchini unaweza kutoweka iwapo
hawatailinda misingi hiyo.
Akifungua mkutano huo uliowakutanisha viongozi
wakuu wa Serikali waliopo na wastaafu, viongozi wa dini, wazee na
viongozi wa vyama vya siasa, Dk Salim alisema: “Katika kuimarisha amani,
umoja na mshikamano Watanzania tuache ubaguzi na kubaguana kwa hisia za
kiitikadi, dini, ukabila, mahali mtu anatoka, kazi anayofanya au uwezo
wake kiuchumi.
“Na kamwe tusifikiri kuwa amani na umoja ni vitu
ambavyo vipo tu… ukiona kuna amani na umoja ujue kuwa zilifanywa
jitihada, tena jitihada za kweli kweli.”
Alisema kwa kuwa lengo la vyama vya siasa ni
kutawala, haiwezekani kuwa na utawala bora bila kuwa na amani, umoja na
mshikamano katika jamii.
“Tanzania ikipata matatizo hakuna atakayepona.
Biashara haiwezekani katika mazingira ambayo nchi haina amani na
utulivu; kilimo na ufugaji haviwezekani penye fujo,” alisema Dk Salim
ambaye pia amewahi kuwa katibu mkuu wa Umoja wa Nchi Huru za Afrika
(OAU).
Jaji Warioba
Akizungumza katika mkutano huo, Jaji Warioba
alisema hivi sasa jamii imetawaliwa na udini, ukabila na ukanda na
kwamba hata viongozi hawataki kuitwa ‘ndugu’ kama ilivyokuwa enzi za
utawala wa Mwalimu Julius Nyerere.
“Maneno kama ndugu yalikuwa yanaleta usawa, leo
ukimwita kiongozi ndugu anaona umemdharau,” alisema Jaji Warioba na
kuongeza kuwa Serikali ya awamu ya kwanza ilitaifisha shule za dini ili
kuleta usawa na umoja lakini hivi sasa hali hiyo imeanza kuondoka.
Comments
Post a Comment