Rais aipasua kichwa Ukawa 2015
Reported by: HENRY MWALWALA
Kutekeleza hilo, Jumapili iliyopita wenyeviti wa vyama hivyo, Profesa
Ibrahimu Lipumba (CUF), Freeman Mbowe (Chadema), James Mbatia (NCCR-
Mageuzi) na Dk Emmanuel Makaidi (NLD) walisaini makubaliano ya
ushirikiano huo katika mkutano mkubwa wa hadhara uliofanyika Viwanja vya
Jangwani.PICHA|MAKTABA
Dar es Salaam. Baada ya vyama
vinne vya upinzani nchini kusaini makubaliano ya kushirikiana pamoja na
kusimamisha mgombea mmoja katika chaguzi zote zijazo, umoja huo sasa
unakabiliwa na kazi ngumu ya kuweka sawa mambo, ikiwa ni pamoja na
mchakato wa kumpata mgombea urais, kabla ya filimbi ya uchaguzi
kupulizwa.
Vyama hivyo vitalazimika kufanya uamuzi katika
sera tofauti za vyama vyao, kukabiliana na Sheria ya Uchaguzi, taratibu
za kupata wagombea wa kuanzia ngazi ya chini hadi urais na jinsi ya
kuendesha kampeni zao kabla ya kuwaendea wananchi kuwaeleza kuwa
wameshajizatiti kukabiliana na chama tawala, ambacho kina mtandao karibu
nchi mzima uliojengwa kwa miaka mingi.
Vyama hivyo vimeibuka na nguvu mpya baada ya
kuunganishwa na hoja ya kutetea Rasimu ya Katiba iliyowasilishwa na
iliyokuwa Tume ya Mabadiliko ya Katiba ambayo ilielezewa kuwa ilitokana
na maoni ya wananchi na hivyo kuunda Umoja wa Katiba ya Wananchi (Ukawa)
kupambana na wajumbe wa CCM kwenye Bunge Maalumu la Katiba.
Vyama hivyo, Chadema, CUF, NCCR Mageuzi na NLD
vilisusia mchakato wa Katiba kwa kile vilichodai kuwa ni kutoridhishwa
na mambo yalivyokuwa yakiendeshwa na sasa umoja wao umekwenda mbali
zaidi kutaka kushirikiana kwenye chaguzi.
Kutekeleza hilo, Jumapili iliyopita wenyeviti wa
vyama hivyo, Profesa Ibrahimu Lipumba (CUF), Freeman Mbowe (Chadema),
James Mbatia (NCCR- Mageuzi) na Dk Emmanuel Makaidi (NLD) walisaini
makubaliano ya ushirikiano huo katika mkutano mkubwa wa hadhara
uliofanyika Viwanja vya Jangwani.
Moja ya kazi ngumu inayoukabili umoja huo ni jinsi
ya kumpata mgombea wa urais atakayetoa upinzani mkubwa zaidi kwa
mgombea wa chama tawala na kuendelea kupunguza kura za CCM baada ya
mafanikio ya mwaka 2010 ya kupunguza asilimia 20 za kura alizopata
RaisJakaya Kikwete mwaka 2005.
Kazi hiyo ngumu inatokana na tofauti za kisera
baina ya vyama hivyo, wagombea urais wanaoonekana kuwa na sifa na
matokeo ya uchaguzi uliopita uliompa mgombea wa Chadema, Dk Willibrod
Slaa asilimia 26 ya kura zote na kuweka rekodi ya upinzani kukusanya
kura nyingi.
Wakati Chadema ikitegemea mtaji wa Dk Slaa, ambaye
ni katibu mkuu wa Chadema, wa asilimia 26.34 ya kura za mwaka 2010, CUF
imekuwa ikimsimamisha mwenyekiti wake, Prof Lipumba katika chaguzi nne
zilizopita, huku NCCR-Mageuzi ikiwa na mwenyekiti wake, james Mbatia na
NLD ikiwa na Makaidi.
Mbowe alisema hilo halitakuwa tatizo kubwa katika kufikia uamuzi wa mgombea urais.
“Kwanza niseme tu kuwa hapa tulipofika haikuwa
rahisi sana kama watu wanavyodhani, kwa hiyo yako mengi ambayo
yamefanyika kwa kujadiliana na katika mchakato huu tumejifunza mengi.
Kwa hiyo taratibu zitawekwa na zitafuatwa. Kutakuwa na vigezo na mambo
kama hayo,” alisema mwenyekiti wa Chadema Freeman Mbowe alipozungumza na
gazeti hili mwishoni mwa wiki akijaribu kuonyesha kuwa wamezingatia
mambo mengi kabla ya kusaini makubaliano hayo.
“Suala la mgawanyo wa nafasi za kugombea haliwezi
kutugombanisha. Ushindani si jambo geni kwetu maana tumekuwa na
ushindani siyo sasa tu, bali hata ndani ya vyama. Hata katika chama
kimoja huwa kuna wagombea zaidi ya mmoja.”
Kauli ya Mbowe iliungwa mkono na Mbunge wa Kigoma
Kusini (NCCR-Mageuzi), David Kafulila ambaye alisema ili kuondoa utata
wowote unaoweza kujitokeza, kamati ya ufundi itaundwa kwa ajili ya
kushughulikia masuala yote muhimu.
Comments
Post a Comment