Serikali mbili hazitaruhusu kupatikana Katiba mpya-CUF


25th August 2014

Naibu Katibu Mkuu wa chama hicho, Nassor Ahmed Mazrui
Chama cha Wananchi (CUF) kimesema katiba mpya haiwezi kupatikana kwa sababu matatizo ya Muungano yaliopo katika mfumo wa serikali mbili haufai na unahitaji marekebisho makubwa.

Kauli hiyo imetolewa na Naibu Katibu Mkuu wa chama hicho, Nassor Ahmed Mazrui, na kwamba kitendo cha kung’ang’ania mfumo uliopo sasa wa Serikali mbili ni chanzo kitakachopelekea kifo cha  Muungano kwa sababu hakuna ufumbuzi wa kero hizo.

“Hatuwezi kupata katiba ya aina yoyote kama tutaendelea kuwapo kwa mfumo wa Muungano wa Serikali mbili ambao tafiti mbalimbali zimeonyesha bayana kwamba haufai,” alisema Mazrui.

Alisema Tume mbalimbali zilizoundwa kuangalia mwenendo wa Muungano pamoja na ripoti za utafiti za wasomi mbalimbali ambao wengine ni mawaziri wa Serikali ya Muungano zimekuja na ripoti inayoonyesha kwamba Muungano bora wenye maslahi kwa pande zote mbili ni wa Serikali tatu.

Alisema kinachofanywa sasa katika Bunge maalumu la katiba ni kama mchezo wa kuigiza mhusika mkuu wa mchezo huo ni CCM.

“Mimi siku zote nasema watu watakaovunja Muungano huu ni CCM ambao ndiyo wa kulaumiwa kwa sababu hawapo tayari kukubali maoni na marekebisho ya mfumo wa Muungano uliopo sasa,” alisema Mazrui.

Alisema CUF ambayo inaunda Umoja wa  Katiba ya wananchi (Ukawa) hawawezi kurudi katika Bunge hilo kwa kwenda kuhalalisha matatizo ambayo watakaobeba mzigo huo ni wananchi.

Mazrui ambaye ni Waziri wa Biashara Viwanda na Masoko wa Serikali ya Umoja wa Kitaifa, alisema Wazanzibari wanahitaji mfumo wa Muungano utakaokuwa na maslahi nao ambao utaondoa kero ziliopo sasa  zikiwamo za kiuchumi na maendeleo.
 

Comments

UNITEC COMPUTER ACCESS